Sunday, November 6, 2011

Ansbert Ngurumo: Muone, kichwa kama CCM

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjs8wny5CiVKPSiBZBLde2ff4-7J8B3crcl7ur2AZxjnUNYPwe98GqaQxCR2XiaGBBJYsOl_rigN8RqJJVetWZnB3n5uyqbb6lkKBBQaIOXXfJjQBZwLA5SUPyOHVMuygeNIJJFhbBJeoTr/s220/Ansi+13.11.2007.bmp
NAWAHUSUDU, na wakati mwingine nawashangaa sana Watanzania wenzangu wanaojipanga kuomba uongozi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hawa ni watu waliojilipua. Wanahitaji nguvu ya ziada.
Maana zama zimebadilika. CCM sasa kimekuwa mzigo mzito usiobebeka kwa kila Mtanzania.
Hata viongozi wa chama, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, wameanza kutambua kwamba kuongoza CCM si jambo la kujivunia tena. Ni changamoto kubwa sana. Ni adhabu!
Wanachama nao wamefika mahali wanaona aibu kujitambulisha kama wana CCM, kwa sababu wanaogopa kuzomewa. Siku hizi, ukitaka kulinda heshima yako, fiche u-CCM wako.
Baadhi ya makada maarufu, wakiwamo wabunge, wamekiri kwangu kwamba katika maeneo mengi ya nchi hii, chama hakiuziki, hakibebeki. Wanasisitiza kwamba tofauti na zamani ambapo chama kilikuwa nyenzo muhimu inayotumika kuwabeba wanasiasa wanaogombea uongozi, sasa hivi imefika mahali ambapo wagombea ndio wanatarajiwa kukibeba chama.
Maana yake ni kwamba ukitaka kugombea uongozi CCM lazima uwe na pesa nyingi za kuhonga wananchi na kununua ushindi, na uwe na uhakika wa kuitumia dola dhidi ya wapinzani wako.
Ni siri iliyo wazi kwamba wabunge wengi wa CCM waliochaguliwa mwaka jana, walipita kwa sababu ya majina yao, na jitihada binafsi; si kwa sifa ya chama.
Baadhi ya wale niliozungumza nao, wamekiri kwamba katika majimbo yao, wao ndio CCM – maana ndio wanaokibeba chama badala ya chama kuwabeba wao. Mmoja wao aliniambia kwamba ingawa yeye ni mbunge wa CCM, ana uhakika kwamba pale jimboni kwake hakuna CCM, bali kuna CHADEMA.
Maana yake ni kwamba wabunge hao wangechaguliwa tu, hata kama wangegombea kupitia chama kingine.
Tafsiri ya haraka ni kwamba iwapo wabunge hao wa CCM wakihama chama leo, wataondoka na wapiga kura wao.
Na hii ndiyo tofauti kubwa ya sasa kati ya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mbele ya umma.
Kwa asilimia kubwa, chuki ya wananchi dhidi ya CCM imegeuka ushabiki na mapenzi kwa CHADEMA. Pale ambapo kada au mgombea wa CCM anaona aibu kujinadi kwa chama chake, yule wa CHADEMA anajua kuwa asipotumia mwamvuli wa chama kujinadi anakuwa na nafasi ndogo ya kushinda.
Ile jeuri ya wanachama na mashabiki wa CCM kutembea kifua mbele wakiwa wamevaa mashati na fulana na kijani na njano mitaani, imenyauka.
Ndiyo maana kada mmoja wa CCM aliyekuwa mstari wa mbele katika uchaguzi mdogo wa Igunga aliniambia kuwa ilifika mahali wakagundua kwamba kijani chao ni nuksi, kinachukiwa na kitawanyima fursa ya kufanya kampeni kwa amani.
Akasema, “Tuligundua hilo, tukawa hatuvai mashati na fulana za kijani, bali tunavaa kiraia, ndipo tunapata uhuru wa kupita mitaani na kuomba kura nyumba kwa nyumba.”
Hii ndiyo sababu inayowafanya CCM kuandaa mikutano ya hadhara kwa gharama kubwa mno, ikuhusisha kubeba wananchi kwenye malori na mabasi kutoka sehemu za mbali na kuwaleta mahali pa mkutano, tena baada ya kuwaahidi au kuwagawia pesa au fadhila nyinginezo.
Ndiyo maana vijana waendesha pikipiki na daladala hawaendi kwenye mikutano ya CCM kwa hiari. Lazima wahongwe mafuta na kupewa pesa ya kula; wakati vijana hao hao hushindana wao kwa wao kununua mafuta na kujaza matanki ya pikipiki au magari yao kwenda kwenye maandamano na mikutano ya CHADEMA.
Hiii ni sehemu ya maelezo kwa nini CCM hawawezi kushinda bila kutegemea nguvu ya pesa na polisi. Wakati tuliomo ni ule wa chama tawala kuishi kwa kudra za dola, huku upinzani ukikua kwa kasi ya ajabu kwa kudra za nguvu ya umma.
Miaka kadhaa iliyopita, katika maeneo mengi ya nchi hii, ilikuwa aibu na kejeli mtu kujinadi kuwa mpinzani. Sasa hivi ni jambo lisilo la kujivunia mtu kujitambulisha hadharani kuwa ni mwana CCM.
Miaka saba iliyopita, wananchi kadhaa huko vijijini waliwahi kuniambia kuwa mtu anayetamani kugombea uongozi, kama ana nia ya kushinda apitie CCM.
Mwaka huu, wananchi wale wale wamenieleza kwamba kama mtu anataka kushindwa agombee kwa tiketi ya CCM.
Kama ambavyo baadhi yetu tumesema huko nyuma, CCM kinakufa. Hata hiyo idadi ya wanachama wanayotangaza, milioni nne, haipo. Ni propaganda tu za kisiasa.
Ikumbukwe kuwa waasisi wa CCM wanazidi kufa. Wengine wanazeeka. Wengine wamekihama chama. Sehemu kubwa ya idadi ya Watanzania ni vijana. Ni wao wamezaliwa miaka ya harakati za mageuzi ya kisiasa. Wengi wao wamejiunga kwenye vyama vya mageuzi. Sasa hivi hata watoto wadogo wanasalimiana kwa kunyosha vidole viwili, ishara ya ushindi inayotumiwa CHADEMA.
Shule za sekondari na vyuo vya elimu ya kati na ya juu vimejaa wanafunzi wasiokipenda CCM. Katika mazingira haya, CCM kinazidi kukosa mvuto, na wanachama wa CCM wanazidi kupungua.
Kinawapata wapi hao milioni nne? Kama kina wanachama wengi hivyo, mbona hawakubali kuhudhuria mikutano ya CCM bila kubembelezwa na kuhongwa?
Kama CCM kingekuwa na idadi kubwa kiasi hicho, CHADEMA kingepata wapi jeuri ya nguvu ya umma?
Chuki ya wazi dhidi ya CCM inasababishwa na maisha magumu waliyonayo wananchi. Udhaifu wa serikali ndio umekiua CCM, maana kimegeuka chama cha viongozi waongo, wasioaminika.
Mwaka huu, wakati tunatimiza miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, tunatimiza pia miaka sita ya utawala wa Rais Kikwete.
Ni miaka sita ya shida na umaskini unaosababisha chuki ya wananchi dhidi ya Rais Kikwete. Hatujasahau kwamba mwaka 2005 Kikwete aliomba kura akiahidi maisha bora kwa kila Mtanzania. Yako wapi?
Utafiti uliofanywa na taasisi ya takwimu, ya serikali hii hii, kuhusu mapato binafsi ya kaya, unaonyesha kuwa mwaka huo (2005) Watanzania waliokuwa wanakula mara moja tu kwa siku walikuwa asilimia 34 ya wananchi wote.
Mwaka huu, idadi ya Watanzania wanaobahatisha mlo mmoja tu kwa siku imeongezeka hadi asilimia 41. Maana yake, idadi ya Watanzania wanaoshinda au kulala njaa katika miaka mitano ya Rais Kikwete imeongezeka kwa asilimia saba!
Hawa wana sababu ya kuiamini CCM? Wana sababu ya kuipenda CCM? Wana sababu ya kuiamini serikali ya Rais Kikwete? Wameyaona maisha bora waliyoahidiwa na JK?
Utafiti huo huo unaonyesha kuwa asilimia 42 ya watoto wote wenye miaka mitano katika kipindi hichi hicho wamedumaa. Kama wazazi wao wanakula mara moja tu kwa siku, tena kwa kubahatisha, watoto wao watawezaje kukua vizuri na kupata maisha bora? Wazazi wa watoto hawa waliodumaa wana sababu za kushangilia miaka 50 ya utawala wa CCM na sita ya maisha magumu ya JK?
Taifa la watoto waliodumaa linajivunia miaka 50 ya CCM na sita ya Kikwete? Taifa la namna hii linaona manufaa ya kuongozwa na CCM yenye magamba au isiyo na magamba?
Takwimu hizo hizo za serikali zinaonyesha kuwa katika kipindi kile kile walichoahidiwa maisha bora, asilimia 54 ya Watanzania wote hawali nyama kabisa!
Tutawezaje kujivunia afya na usitawi wa watu wetu kama wanakosa hata virutubisho muhimu kama protini itokanayo na nyama?
Hii ina maana gani kwa taifa linalosemekana kuwa la tatu kwa wingi wa mifugo katika Afrika, ambalo zaidi ya nusu ya watu wake hawali nyama?
Mambo haya na mengine ndiyo yamewafanya baadhi ya watu kuogopa kujitambulisha kuwa wana CCM.
Na sasa nimesikia katika baadhi ya maeneo nchini, CCM imegeuka tusi miongoni mwa vijana. Ukimuudhi mtu siku hizi, akakosa tusi la kistaarabu dhidi yako, atakwambia: “Muone, macho kama CCM!”

No comments:

Post a Comment